Wednesday, 24 September 2014
WACHUNGAJI WALAWITI WATOTO, ARUSHA
Watoto sita, wakiwemo wawili wa kiume wenye umri wa miaka 8 hadi 14 wameharibiwa vibaya sehemu zao za siri baada ya kubakwa kanisani na watu wanaodaiwa ni wachungaji.
Watoto sita waliobakwa kanisani na watu wanaodaiwa ni wachungaji.
Wakiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru walikopelekwa kwa matibabu na kuangaliwa maambukizi ya magonjwa ya zinaa, watoto hao walidai kufanyiwa mchezo huo kwa nyakati tofauti na wachungaji watatu wa kanisa hilo lililopo eneo la Field Force, Kwamorombo jijini Arusha.
Mmoja wa watoto hao anayesoma darasa la 4 katika shule ya msingi alieleza kuwa yeye na wenzake wamekuwa wakifanyiwa mchezo mchafu katika kanisa hilo baada ya wachungaji hao kuwapatia shilingi 2,000 za kufungia mdomo.
“Siku moja nilipofika shuleni wenzangu wakaniambia niende pale kanisani tukapewe hela, nilipofika niliwaona wenzangu wengine wakifanyiwa mchezo mchafu na mimi mchungaji aliniambia niiname akanifanyia kitendo kibaya na kunipa shilingi 2,000, niliumia sana,’’ alisema mwanafunzi mmoja.
Tuesday, 23 September 2014
SHAIRI - BINGWA AMETOKA KAPA
Alileta zake mbwebwe, Na mashabiki lukuki
Akasema hata Wembe, Ukiletwa hakatiki
Yeye anakula sembe, Wali kwake hashituki
Bingwa ametoka kapa, Aso bingwa hali gani?
Akaivaa na jezi, Ugani akajitosa
Na kuwaita Malezi, Wale walokula kasa
Kumbe vile hajiwezi, Ni lijoka la kipisa
Bingwa ametoka kapa, Aso bingwa hali gani?
Aliposhindwa ugani, La kusema alikosa
Kusingizia utani, Kumbe vile ni garasa
Walikwama wa maini, We utumbo ndo kabisa
Bingwa ametoka kapa, Aso bingwa hali gani?
Unapokwenda mechini, Muhimu ujizatiti
Usijitie kundini, Na kuleta tashtiti
Ukija bila plani, Utarudi umaiti
Bingwa ametoka kapa, Aso bingwa hali gani?
Shairi hili limeandikwa na Wazir Khamsin
WAPIGANAJI WA IS WATOA VIDEO YA PILI
Video ya pili imetolewa ikimwonyesha mwandishi wa habari wa Uingereza John Cantlie, ambaye anashikiliwa mateka na wanaojiita wapiganaji wa IS.
Tukio hilo linatokea wiki moja baada ya kutokea kwenye video kufuatia kutekwa kwake nchini Syria mwaka 2012.
Akiwa amevalishwa mavazi ya rangi ya machungwa, Bw Cantlie amesema ametelekezwa na Uingereza.
Hivi karibuni IS iliwaua mateka watatu na, kwenye video ikionyesha kifo cha mfanyakazi wa kutoa misaada wa Uingereza David Haines, na huku wakitishia kuua raia mwengine wa Uingereza Alan Henning
Ni mwandishi wa habari mwenye uzoefu mkubwa, hii ni mara ya pili kwa Bw Cantlie kutekwa Syria.
Aliwahi kutekwa Julai 2012, kufungwa pingu na kufungwa macho kwa wiki nzima, alifanikiwa kutoroka akisaidiwa na wapiganaji wanaojiita Free Syrian Army.
Video hii ya hivi karibuni imekuwa ikisambazwa huku Marekani na washirika wake wakianzisha mashambulio ya anga dhidi ya IS nchini Syria.
Majeshi ya Uingereza hayajajihusisha lakini serikali imesema huenda ikajihusisha siku za usoni.
Video hiyo ya takriban dakika sita, inafuatia mbinu zilezile za video ya kwanza akiwemo mwandishi wa habari.
Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
MAMBO 10 YALIYOTIKISA BUNGE, TANZANIA
Hata hivyo hali ilikuwa kinyume katika hitimisho, baada ya wajumbe hao waliokuwa wakitaka kura ya siri kugeuka na kupiga kura ya wazi licha ya kuwa uhuru ulitolewa wa aina mbili za kura.PICHA|MAKTABA |
Hakuna marefu yasiyo kuwa na ncha, ni usemi wa zamani wa wahenga wenye maana ya kila jambo lenye mwanzo, lazima litakuwa na mwisho.
Ndivyo ilivyo kwa Bunge la Katiba ambalo safari yake ilianzia Februari 18 mwaka huu na kutarajia kuhitimishwa Oktoba 4 kwa ajili ya kutoa Katiba inayopendekezwa.
Yapo mengi yaliyofanyika ndani ya Bunge hilo yakiwamo mazuri yaliyofurahisha masikioni mwa watu, licha ya kuwa kuna baadhi ya mambo yaliyotoa tafsiri hasi kwa makundi yote.
Mbali ya hayo, ziko ndimi ambazo zilipasua Bunge hilo na hata wakati mwingine kusababisha mivutano mikali kiasi cha kuleta mkanganyiko uliotafsiriwa kivingine.
Kikubwa ni kuwa, sasa mchakato huo unafikia mwisho ili ipatikane Katiba inayopendekezwa ambayo itawekwa kabatini ikisubiri rais ajaye ambaye ataanzia kura ya maoni kwa wananchi baada ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
Mjadala wa Bunge hilo ulitikiswa na mengi lakini kumi ndiyo hasa yalionekana wazi kuleta mvutano mkali kiasi cha kuligawa Bunge hilo ikiwamo suala la kura ya wazi au kura ya siri.
Monday, 22 September 2014
ETIHAD YAANZA SAFARI ZA DAR ES SALAAM
Etihad Airways, ndege ya taifa ya UAE itapanua safari zake za barani Afrika kwa kuanzisha safari za kila siku mjini Dar es Salaam, mji mkubwa kuliko wote Tanzania.
Safari za ndege baina ya Abu Dhabi na Dar es Salaam, zitakazoanza tarehe 1 Desemba 2015, zitafanyika kutumia ndega aina ya Airbus A230 ikiwa na viti 16 vya daraja ya Business na viti 120 vya daraja ya Economy.
Dar es Salaam itakuwa nchi ya 110 duniani kufikiwa na Etihad Airways, na nchi ya 11 barani Afrika na eneo la Bahari ya Hindi.
Safari hiyo ya kila siku itapitia Abu Dhabi, na safari za kuunganisha kwenda mataifa maarufu 45 kupitia Mashariki ya Kati, Ulaya, maeneo ya kusini mwa India, Kaskazini na kusini-mashariki mwa Asia na Australasia.
Matumaini makubwa ni kuwa njia hizo mpya za safari zitaongezwa nguvu na wasafiri wengi wanaofanya biashara na waendao likizo, pamoja na ukubwa wa mizigo, kati ya maeneo ya Afrika Mashariki, maeneo ya kusini mwa India pamoja na China.
RAIS MUSEVENI KUWEKEWA VIZINGITI NA WAPENZI WA JINSIA MOJA, MAREKANI
Rais Yoweri Museveni wa Uganda |
Kundi la wapenzi wa jinsia moja Dallas, Texas, Jumatano iliyopita walizilamisha hoteli mbili kumkatalia Rais Museveni kukaa, kwa madai kuwa ni mkiukaji wa haki za binadamu.
Kulingana na wavuti ya haki za wapenzi wa jinsia moja dallasvoice.com, Rais alishapanga kufikia hoteli ya Four Seasons huko Irving na baada pia ya kupanga Raylard Texan Resort na Convention Center napo alikataliwa baada wapenzi hao inavyodaiwa kupiga simu chungu nzima, wakitaka hoteli hizo zisimpokee.
"Watu wangu walinipangia hoteli, lakini hawa wapenzi wa jinsia moja wamezuia. Nikasema waambie hao watu walionialika kunitafutia sehemu ya kulala. Sio kwamba nina usongo wa kuja Texas." Bi Sarah Kagingo, msaidizi maalum wa Museveni anayesimamia mitandao yake ya kijamii alimnukuu Rais huyo kwenye taarifa iliyotolewa.
Hatahivyo, kulingana na Bi Kagingo, Rais huyo baadae alipangiwa hoteli nyingine - Howdy Lone Star Ranch huko Texas.
Bw Museveni alikuwa akikutana na Waganda waishio nchi za nje siku ya Jumapili, Texas kujadili uwezekano wa kuwekeza na kuchangia katika ukuaji wa kiuchumi Uganda.
Rais huyo aliwahakikishia wawekezaji kuwa ameandaa mpango kupitia nyanja mbalimbali kurahisisha uwekezaji nchini humo.
Chanzo: Daily Monitor, Uganda
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
NJUGU ZILIZOKAANGWA ZINA ATHARI ZAIDI YA MBICHI
Njugu zilizokaangwa haziliwi sana Asia Mashariki, ambapo mzio wa njugu ni nadra sana kutokea huko |
Njugu au karanga zilizokaangwa zina uwezekano mkubwa wa kuibua mzio (allergy) kuliko zilizo mbichi, kulingana na utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Oxford, wakihusishwa panya.
Wanasayansi wanasema mabadiliko ya kikemikali yanayosababishwa na mchakato huo wa kukaanga hubadili mfumo wa kinga wa mwili - na kuibua mzio.
Lakini utafiti zaidi unahitajika kabla watu kuamua kula njugu mbichi zaidi kuliko zilizokaangwa, walisema.
Utafiti huo unapatikana kwenye jarida la Allergy and Clinical Immunology.
Madhara makubwa
Panya walifanyiwa utafiti wa kuwekewa protini za njugu kupitia kwenye ngozi na tumboni mwao.
Wale waliopewa karanga mbichi walikuwa na kinga zaidi ya mwili - waliweza kupambana na vitu vya kigeni mwilini mwao, kuliko wale waliokula zile zilizokaangwa.
Kwa binadamu, namna kinga za mwili zinavyopambana hutofautiana. Wengine kinga zao za mwili ni za wastani na kusababisha vipele kwa mfano, lakini wengine huathirika zaidi, ambapo huvimba midomo na hata kupata matatizo ya kupumua.
Wanasayansi wanasema uwezekano mkubwa ni kutokana na jotoridi kuongezeka wakati wa kukaanga njugu ambapo husababisha mabadiliko ya kikemikali na ndipo mtu huathirika na mzio.
MBINU YA KUZUIA EBOLA YAFANIKIWA, SIERRA LEONE
Mitaa ya Freetown ilikuwa haina watu kabisa wakati wa amri ya kutotoka nje ilipotolewa |
Amri ya kutotoka kwa siku tatu kwa nia ya kuzuia kuenea kwa mlipuko wa Ebola nchini Sierra Leone imetangazwa kufanikiwa na serikali.
Amri hiyo ilisitishwa usiku wa Jumapili na haitosogezwa, serikali ya nchi hiyo imesema.
Sierra Leone ni miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi na mlipuko huo, huku zaidi ya waathirika 550 miongoni mwa 2,600 kwa jumla wakiwa wameripotiwa kuathirika.
Wakati huohuo, nchi jirani ya Liberia imetangaza kuongeza vitanda kwa wagonjwa hao wa Ebola.
Liberia ndio nchi iliyoathirika zaidi na ugonjwa huo, ikiwa zaidi ya nusu ya idadi ya wote waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo wakitoka nchini humo.
Mlipuko wa Ebola Afrika magharibi ni mbaya kuwahi kutokea eneo hilo, Shirika la Afya duniani WHO limesema. Kirusi cha ugonjwa huo huenezwa kwa jasho, damu na mate, na hakuna tiba iliyothibitishwa hadi sasa.
Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
Sunday, 21 September 2014
NYUMBA MPYA YA BIG BROTHER YAPATIKANA
Nyumba mpya ya Big Brother
imepatikana mjini Johannesburg, Afrika kusini, kufutaia moto mkubwa uliozuka na kuteketeza kabisa nyumba ya awali tarehe 2 Septemba.
M-Net na waandaaji wa Big Brother Endemol wamethibitisha hilo, sehemu ya tisa katika kipindi hicho cha televisheni ambacho hurushwa moja kwa moja kitaanza kuonyeshwa tarehe 5 Oktoba, ambacho kitaitwa Big Brother Hotshots.
Kipindi hicho kilitakiwa kianze tarehe 7 Septemba, chenye washindani kutoka nchi 12 za bara la Afrika tayari wakiwa katika hoteli mbalimbali mjini Johannesburg wakiwa tayari kuingia kwenye nyumba hiyo.
Lakini katika tukio la ajabu, taarifa ziliibuka ghafla Afrika kuwa nyumba hiyo imewaka moto, na kipindi hicho kusogezwa mbele.
Msako wa kutafuta nyumba nyingine ukaanza, huku wanaoandaa kipindi hicho wakianza kufikiria mbadala wa kurusha kipindi hicho nchi nyingine ya Afrika, kufuatia wito kutoka kwa wapenzi wa kipindi hicho kiwape nafasi nchi nyingine kuandaa.
Awali, washiriki kutoka nchi 14 za Afrika walitakiwa kuwepo, lakini kutokana na matatizo kwenye hati za kusafiria kutoka washiriki wa Rwanda na Sierra Leone, nchi hizo mbili zikafutwa na kubaki nchi 12.
Iwapo kuchelewa kuanzakwa kipindi hicho kutawapa nafasi nchi hizo mbili haijajulikana bado.
Mshindi wa Big Brother anatarajiwa kuzawadiwa $300,000
Chanzo: New Vision, Uganda
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
Chanzo: New Vision, Uganda
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
MWAKA SASA SHAMBULIO LA WESTGATE, KENYA
Picha za CCTV zikionyesha mtu mwenye silaha akisaka watu wa kuwashambulia |
Kenya inaadhimisha mwaka tangu shambulio kutokea kwenye eneo la biashara la Westagate, ambapo takriban watu 67 waliuawa.
Kutazinduliwa ishara maalum ya kumbukumbu na maombi maalum huku mishumaa ikiwashwa itafanyika.
Shambulio hilo la Westgate lilidumu kwa siku nne, huku kamera za CCTV zikonyesha wateja wa eneo hilo maarufu la kisasa wenye hofu kubwa wakiwakimbia watu wenye silaha na wengine wakijificha.
Kundi la kisomali la al-Shabab lilisema lilifanya shambulio hilo kufuatia harakati za kijeshi zinazofanywa Kenya nchini Somalia.
Tahadhari kubwa
Siku ya Jumapili, ndugu wa waathirika wataweka mashada katika bustani palipo miti 67 yaliyopandishwa baada ya shambulio hilo.
Dua kutoka imani mbalimbali nazo zitasomwa eneo hilo.
"Tunatarajia familia na marafiki wa waliopoteza ndugu zao kujitokeza na kuwa sehemu ya mchakato huu," Rajes Shah alieyandaa shughuli hiyo alinukuliwa na shirika la habari la AFP.
Siku chache kabla ya kumbukumbu hizi, Kenya iliwekwa katika tahadhari kubwa kwa hofu ya uwezekano wa kuwepo mashambulio mengine na wapiganaji.
PROMOTA ALETA TAFRANI SHOW YA DIAMOND, UK
Mwanamuziki Diamond Platnumz kwa mara nyingine tena usiku wa kuamkia jana alisababisha vurugu kubwa nchini Uingereza baada ya kushindwa kutumbuiza katika ukumbi wa LaFace Club uliopo jijini London.
Hii ni mara ya pili kwa Diamond kusababisha vurugu nchi za ughaibuni baada ya Septemba 1, kusababisha vurugu katika mji wa Stuttgart nchini Ujerumani aliposhindwa kufika kwa wakati ukumbini.
Akizungumza na gazeti hili, shuhuda wa tukio ambaye ni Mtanzania anayefanya shughuli zake nchini Uingereza, Flora Lyimo alionyesha wazi kukerwa na tukio hilo ambalo alieleza kuwa huenda likaharibu sifa ya nyota huyo ughaibuni.
Lyimo ambaye alihudhuria shoo hiyo alisema Diamond alisubiriwa na zaidi ya watu 200 tangu saa sita usiku bila nyota huyo kutokea na ilipofika saa 10:00 alfajiri, ndipo walipoanzisha vurugu kudai kurudishiwa pesa zao.
Shoo hiyo ambayo ilitozwa kiingilio cha pauni 20 sawa na fedha za Tanzania Sh54,280 iliishia kwa dosari ya aina yake baada ya polisi kulazimika kuingilia kati kusimamia urudishwaji wa fedha hizo.
Saturday, 20 September 2014
MAZISHI KWA TEKNOLOJIA
Kifo ni 'biashara' kubwa
Ikiwa zaidi ya watu nusu milioni hufariki dunia Uingereza kila mwaka, biashara ya mazishi inatengeneza takriban dola bilioni mbili katika mapato ya kila mwaka, kulingana na kampuni ya utafiti ya masoko Ibis World.
Takriban makampuni 1,500 huajiri watu 20,105, na mapato yanatarajiwa kuongezeka kwa 4.7% kufikia mwisho wa mwaka 2014, kutokana na ongezeko la ushindani wa eneo la kuzika na ndivyo idadi ya watu wanaotaka kuchomwa inaongezeka.
Kukiwa na soko kubwa na lenye faida kubwa, haishangazi kuona makampuni ya teknolojia yamekuwa yakitolea macho huduma za mazishi.
Usia wa Video
Usia wako wa mwisho, kwa mfano ni programu tumishi ya iphone "app" inayomruhusu yoyote kuweka ujumbe wa mwisho kwa wapendwa wao kwa njia ya "usia wa video" ambao utaonekana wakishafariki dunia.
Unatengeneza na kupakua video binafsi yenye usia na halafu unakuwa na neno lako la siri QR code – Ni bar code inayosomeka kwenye simu za kisasa – ambayo humpa mtu unayemwamini unayehisi atakuwa hai utakapofariki.
Ukishafariki dunia, mtu huyo uliyemwamini atatia saini kwenye programu tumishi kwa kutumia alama hiyo ya siri na atapata barua pepe itakayokuwa na ujumbe wako wa mwisho. Baada ya hapo ujumbe huo utatumwa moja kwa moja kwa watu wote uliowakusudia.
Kampuni hii inakiri kuwa "katika nchi nyingi, usia kupitia video haiwezi kuwa mbadala wa usia wa maandishi”, lakini kwa malipo ya ziada, Usia wako wa mwisho unatoa fursa kwa video yako kutumika kisheria kwa kile kinachoitwa ”mchakato mwepesi”.
"Kifo bila shaka ni jambo la huzuni lakini halikwepeki katika maisha ya mwanadamu na ni rahisi zaidi kuacha ujumbe wa mwisho au usia kupitia video kuliko njia iliyozoeleka, inayomhusisha mwanasheria na mashahidi,” Wolfgang Gobler, mkurgenzi mkuu na muasisi wa Usia Wako, aliiambia BBC.
Anaamini teknolojia itaendelea kushawishi huduma za mazishi Uingereza na dunaini kote.
"Kutakuwa na biashara nyingi zinazohusiana na mazishi siku za usoni. Nimeshakutana na wengine ambao ndio kwanza wanaanza huduma hizo za maisha na vifo," amesema.
Chanzo: BBC.
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
SARKOZY ATANGAZA KUREJEA SIASA ZA UFARANSA
Aliyekuwa Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ametangaza kurejea katika siasa.
Katika ukurasa wake wa Facebook, alisema atagombea uongozi wa chama cha upinzani UMP, ikionekana zaidi kama hatua moja mbele katika kugombea urais mwaka 2017.
"Mimi ni mgombea wa kuwa Rais wa familia yangu ya kisiasa," Bw sarkozy aliandika.
Taarifa hiyo inatuliza miezi ya hisia juu ya nia ya mgombea huyo mwenye umri wa miaka 59 wa chama cha Conservative, ambaye aliapa kuacha siasa baada ya kushindwa kuchaguliwa upya nafasi ya urais mwaka 2012.
Uchaguzi wa chama cha UMP unatarajiwa kufanyika mwezi Novemba.
SMZ: HAKUNA MWENYE UBAVU WA KUIPORA PEMBA
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein |
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema Kisiwa cha Pemba ni miliki ya Zanzibar na sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuna nchi yoyote yenye ubavu wa kukichukua kisiwa hicho, imeelezwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumzia mvutano wa mipaka uliojitokeza katika usawa wa Bahari ya Hindi kwenye mwambao wa Somalia na Kenya na kulihusisha eneo la Pemba ikielezwa kuwa ni sehemu ya Kenya.
Kauli ya Waziri huyo imekuja baada ya hivi karibuni kuripotiwa kuwa Somalia imeishtaki Tanzania katika Mahakama ya Kimataifa kuwa inakalia Kisiwa cha Pemba ambacho ni mali ya Kenya.
Vilevile Somalia imeishtaki Kenya katika mahakama hiyo na kwamba nayo iko katika hatari ya kupoteza umiliki wa visiwa katika Pwani ya Bahari ya Hindi.
Aboud alisema mipaka ya nchi inaonyesha wazi Kisiwa cha Pemba kimekuwa ni sehemu ya Zanzibar na hakuna sababu ya kulitilia shaka jambo hilo kuhusu mvutano uliojitokeza baina ya mataifa hayo na kuamua kufungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa.
MUASI WA KIKE WA LIBERIA AKAMATWA
Charles Taylor alituhumiwa kwa kufanya ukatili wa hali ya juu |
Makundi ya kutetea haki za binadamu yamefurahishwa na kukamatwa kwa kamanda wa kike wa muasi Charles Taylor nchini Belgium kwa uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanyika wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe Liberia.
Kukamatwa huko kumefanyika baada ya malalamiko kuwasilishwa kwa niaba ya watu watatu walioathrika kwenye mapigano mwaka 1992 iliyojulikana kama Operation Octopus.
Martina Johnson bado hajasema chochote juu ya madai ya kuhusika na "ukataji viungo na mauaji ya watu wengi".
Bw Taylor amefungwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita yaliyofanyika nchi jirani ya Sierra Leone.
Mahakama maalum iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilimkuta na hatia mwaka 2012 kwa usambazaji wa silaha kwa waasi wa Sierra Leone na badala yake kupewa kile kilichoitwa almasi haramu 'blood diamond'.
Alianzisha uasi nchini Liberia mwaka 1989, na kuwa Rais mwaka 1997- lakini alilazimika kukimbilia uhamishoni baada ya mapigano na kundi jengine la uasi mwaka 2003.
Friday, 19 September 2014
RAIS KENYATTA WA KENYA ATAKIWA ICC
Kesi dhidi ya Uhuru Kenyatta imewakasirisha viongozi wengi wa Afrika |
Mahakama ya Kimataifa ya ICC imemtaka Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta afike katika mahakama hiyo tarehe 8 Oktoba.
Majaji wanataka kumhoji juu ya madai kuwa serikali yake imeshikilia nyaraka zinazotakiwa na waendesha mashtaka wanaoandaa kesi yake ya uhalifu dhidi ya binadamu.
Kesi hiyo tayari ishacheleweshwa mara tele.
Bw Kenyatta anakana kuhusika na mauaji ya kikabila baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Takriban watu 1,200 waliuawa na 600,000 kulazimika kuhama makazi yao.
Wiki mbili zilizopita, waendesha mashtaka waliomba kesi dhidi yake iahirishwe bila kutaja tarehe gani isikilizwe tena, wakisema hawana ushahidi wa kutosha kutokana na serikali ya Kenya kuchelewesha kutoa taarifa.
Rais Kenyatta amekuwa akisema mara kwa mara kuwa anahitaji kubaki Kenya ili kupambana na wapiganaji wa kundi la al-Shabab na kushughulikia masuala ya taifa.
Katika taarifa iliyotolewa, ICC imesema mazungumzo na Bw Kenyatta yatalenga " hali ya ushirikiano baina ya upande wa mashtaka na serikali ya Kenya".
Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
WAZIRI MKUU UGANDA AFUKUZWA NA RAIS MUSEVENI
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uganda Amama Mbabazi |
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amemfukuza kazi waziri wake mkuu Amama Mbabazi.
Nafasi yake sasa inachukuliwa na Ruhakana Rugunda, ambaye kabla ya kuteuliwa alikuwa waziri wa afya.
Bw. Mbabazi amekuwa mshirika wa karibu wa Rais Museveni lakini wachambuzi wanasema ushirikiano wao umekuwa ukizorota.
Mapema mwaka huu chama tawala nchini humo kilimpitisha Rais Museveni kuwa mgombea pekee wa Urais mwaka 2016 lakini inaelezwa kuwa Bw Mbabazi alipinga uamuzi huo.
MWANASIASA WA ZIMBABWE AFA KANISANI
Mwanasiasa wa Zimbabwe wa upande wa upinzani ni miongoni mwa watu 80 waliofariki dunia baada ya kanisa moja mjini Lagos, Nigeria kuporomoka wiki moja iliyopita.
Wengi waliofariki dunia kwenye tukio hilo ni raia wa Afrika kusini waliokuwa wakiishi kwenye jengo hilo lenye ghorofa kadhaa linalomilikiwa na kanisa la mhubiri maarufu TB Joshua.
Serikali ilisema ilikuwa na ghorofa nyingi kuliko ilivyoweza kuhimili.
Zaidi ya watu 130 walinusurika, akiwemo mwanamke mmoja wa Afrika kusini aliyetolewa kwenye kifusi siku ya Jumatatu - siku tatu baada ya jengo kuporomoka.
Kifo cha Bw Ndanga kilithibitishwa na familia yake na maafisa wa chama siku ya Alhamisi.
Msemaji wa MDC Douglas Mwonzora alisema Bw Ndanga alikuwa mchungaji na alikwenda Nigeria kwa shughuli za kanisa, limeripoti gazeti la taifa la Zimbabwe, Herald.
USKOCHI YASEMA 'HAPANA' KWA UHURU
Uskochi imepiga kura kubaki kwenye muungano na Uingereza baada ya wapiga kura kukataa uhuru.
Matokeo yakiwa yametoka kwenye manispaa zote 32, kura ya “Hapana” imepata 2,001,926, dhidi ya 1,617,989 waliopiga "Ndio".
Waziri kiongozi wa Uskochi ametoa wito wa kuleta umoja na vyama vya muungano kutoa madaraka zaidi.
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron alisema alifurahi sana kuwa Uingereza itabaki ikiwa imeungana na ahadi za kutoa madaraka zaidi zitaheshimiwa.
Bw Cameron amesema vyama vikuu vitatu vya muungano Westminister sasa vitatekeleza ahadi ya kutoa madaraka zaidi kwa bunge la Uskochi.
"Tutahakikisha ahadi zilizotolewa zitaheshimiwa," alisema.
Alitangaza kuwa Lord Smith, ambaye aliongoza michezo ya Jumuiya za Madola huko Glasgow, atasimamia mchakatao mzima wa kutekeleza ahadi hizo, ikiwemo madaraka mapya juu ya kodi pamoja na matumizi kufikia makubaliano ifikapo mwezi Novemba, na rasimu ya bunge kuchapishwa ifikapo mwezi Januari.
Waziri mkuu naye alisema kuwa watu wa England, Wales na Ireland kaskazini lazima wawe na usemi zaidi kwenye masuala yao wenyewe.
"Huko Wales kuna mapendekezo ya kuipa serikali na bunge la Wales madaraka zaidi na ninataka Wales iwe kiini cha mjadala wa namna Uingereza itaweza kuwajibika kwa mataifa yetu yote ," alisema.
Thursday, 18 September 2014
MTANZANIA AKABILIWA MIAKA 20 JELA, MAREKANI
Alikuwa akiishi maisha ya kipekee kwenye ardhi yenye ufahari na makuu tele, ambayo wengi nyumbani Tanzania wasingewaza kutokea. Amon Rweyemamu Mtaza alionekana kuishi maisha ya juu sana nchini Marekani, ilivyokuwa ikionekana.
Alikuwa na tatizo moja tu: Utajiri wake ulijengwa kwenye misingi ya uongo – kuwalaghai wanaopokea malipo ya uzeeni yaani pensheni. Na sasa hali halisi imemrudia Mtaza mwenye umri wa miaka 38.
Raia huyo wa Tanzania anayeishi Huoston, Texas, anakabiliwa na kifungo cha miaka 20 jela kwa kufanya udanganyifu katika masuala ya kodi akiwa na mshirika.
Imeripotiwa waliwaibia zaidi ya wazee 600 waliokuwa wakilipwa mafao ya uzeeni ambapo walipata zaidi ya dola milioni 1.8 (zaidi ya shilingi bilioni 3)
Shirika la Habari la AP liliripoti kuwa Mtaza alikiri kushiriki katika jaribio la kufanya udanganyifu kupitia mtandao na makosa mawili mazito ya wizi wa utambulisho.
Waendesha mashtaka Houston walisema Mtanzania huyo na mshirika wake ambaye ni mwanamke walihusika katika wizi huo na kuiba utambulisho wa wazee hao waliokuwa walipwe pesa za uzeeni.
Mtanzania huyo alikamatwa Machi 3.
Chanzo: The Citizen, Tanzania
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
Subscribe to:
Posts (Atom)