Wednesday, 4 March 2015
FORBES: DEWJI BILIONEA KIJANA AFRIKA
Mfanyabiashara maarufu nchini na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohammed Dewji (pichani) kwa mara ya kwanza ameingia kwenye orodha ya mabilionea 29, akiwa tajiri kijana kuliko wote barani Afrika.
Jarida la Forbes la Marekani limemtaja Dewji (39), katika nafasi ya 24 ya matajiri wa Afrika akiwa na utajiri wa Dola 1.3 bilioni za Marekani (Sh2.34 trilioni) unaotokana na biashara mbalimbali anazozifanya kupitia kampuni yake ya Mohammed Enterprises (Metl Group).
“Dewji alibadilisha biashara aliyoanzisha baba yake kutoka uuzaji bidhaa na kuwa na viwanda vya Metl,” inasema sehemu ya habari inayomuhusu bilionea huyo Mtanzania iliyochapishwa juzi jioni.
“Alinunua viwanda vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kwa bei ndogo na kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa menejimenti,” inaongeza ripoti hiyo.
Metl ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.
Katika kampuni hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.
Kwa mujibu wa tovuti yake, Metl inaendesha shughuli za uagizaji na usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo, vinywaji na vyakula, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji baiskeli.
Pia inahusika na huduma za simu, fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Dewji anashika nafasi mbili juu zaidi ya kada maarufu wa CCM na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Igunga, Aziz Rostam (50) aliyewekwa nafasi ya mwisho.
Rostam amefungana nafasi ya 26 na mabilionea wa Nigeria, Abdulsamad Rabiu na Femi Otedola wenye utajiri wa Sh1.8 trilioni kila mmoja.
Orodha hiyo ya 29 bora inaoongozwa na bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote akiwa na utajiri wa Dola 15.7 bilioni za Marekani (Sh28.2 trilioni), kiwango ambacho ni mara moja na nusu ya bajeti ya Serikali ya Tanzania ya mwaka 2014/15.
Forbes linamtaja Rostam kuwa na utajiri wenye thamani ya Dola 1 bilioni za Marekani (Sh1.8 trilioni), kiwango ambacho kimebaki pasi na mabadiliko kutoka orodha ya mwaka jana. Rostam anamiliki asilimia 35 ya hisa katika kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Vodacom.
“Anamiliki pia Kampuni ya Ukandarasi ya Madini ya Caspian ambayo hutoa huduma kwa kampuni kubwa za madini kama BHP Billiton na Barrick Gold (Accasia Gold),” ilibainisha habari hiyo. “Caspian inamiliki pia kampuni nyingine za dhahabu, shaba na chuma, Tanzania,” iliongeza.
Jarida hilo lilibanisha kuwa, Rostam ana miliki nyingine katika Bandari ya Dar es Salaam ambaye yeye ni mbia na Kampuni ya Hutchison Whampoa.
Pia, utajiri wake unatokana na uwekezaji katika tasnia ya maendeleo ya makazi Tanzania, Dubai, Oman na Lebanon.
Ripoti ya Forbes inaenda sanjari na ile ya Jarida ya Ventures Afrika iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana, ambayo iliwataja Dewji na Rostam kuwa ndiyo mabilionea pekee walioingia kwenye orodha ya ‘mabepari’ 55 barani Afrika.
Katika orodha ya ripoti ya jarida hilo, Dewji alikuwa nafasi ya 24, sawa kabisa na anayoshikiria sasa kwenye orodha ya Forbes, akiwa na utajiri wa Dola za Marekani 2 bilioni (Sh3.6 trilioni).
Chanzo: mwananchi.co.tz
Labels:
Habari
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment