Monday, 9 March 2015
MTOTO MWENGINE ALBINO AKATWA KIGANJA TZ
Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ‘albino’ Baraka Cosmas (6) anayeishi na wazazi wake kijijini Kipeta, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga ameshambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana kisha kutokomea nacho kusikojulikana.
Tukio hilo limetokea wakati Serikali ikiwa katika mkakati kabambe wa kupambana na mauaji ya albino na ikiwa ni wiki chache tu tangu mtoto mwingine Yohana Bahati aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja kutekwa Februari 15, mwaka huu na kukutwa ameuawa katika eneo la Shilabela.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema tukio hilo la kikatili lilitokea saa saba usiku wa kuamkia juzi.
Alisema wakati hayo yakitokea baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.
Kamanda Mwaruanda alisema mtoto huyo amelazwa katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa matibabu akiwa pamoja na mama mzazi.
Mwaruanda alisema, “Watu watatu majina yao yamehifadhiwa wanashikiliwa na polisi na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea ili kuwasaka wahusika na kiungo cha mtoto huyo.”
Mama mzazi Prisca Shaaban (28), alisema tukio hilo lilimkutana saa saba usiku, wakati akitaka kutoka nje kujisaidia.
“Nilikutana na mtu akifungua mlango, akanipiga ni kitu kichwani kisha nikazimia, nilipozinduka nikapiga kelele na majirani wakafika ndipo nilipogundua mtoto wangu amekatwa kiganja cha mkono wa kulia,” alisema mama mzazi.
Chanzo: mwananchi.co.tz
Labels:
Habari
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment