Katika nchi nyingi za Afrika, jamii imejigawa katika jamii ndogondogo ziitwazo makabila.
Kila kabila linakuwa na lugha inayotambulisha
jamii ile. Kwa kuwa katika nchi makabila ni mengi na yanaongea lugha
tofauti ambazo mara nyingi hata hazisikilizani, nchi huamua kuweka lugha
moja rasmi kuwa lugha ya taifa.
Wenzetu katika nchi nyingine waliamua kuchukua
lugha ya wale waliowatawala kuwa ndio lugha ya taifa. Hivyo kama
walitawaliwa na Waingereza lugha ya taifa inakuwa Kiingereza, kama
walitawaliwa na Wafaransa basi lugha ya taifa inakuwa Kifaransa.
Tanzania ni nchi moja katika nchi chache sana katika Afrika ambazo
zinatumia lugha ambazo siyo lugha za walio watawala. Sisi Tanzania
tunatumia Kiswahili kama lugha ya taifa.
Mimi najivunia sana lugha hii, ninatamba mbele za
walimwengu kwamba sisi tuna lugha ya Kiswahili inayotuunganisha kama
taifa. Pamoja na kwamba sasa Kiswahili kimeenea sehemu nyingine za dunia
hii hasa zile za Afrika Mashariki bado mimi naona hiyo ni lugha yetu
sisi na wengine wamejifunza kama sisi tunavyojifunza lugha za watu
wengine.
Ninaamini wapo wenye fikira kama hizi za kwangu
lakini ninahisi pia wapo wanaoona lugha hii haiwahusu. Wengi wa hao ni
watu wanaojua Kiingereza ambao wanaona Kiingereza ndiyo utambulisho wa
usomi.
Hivyo hata kama Kiswahili kinadidimia hilo sio
tatizo kwao kwani hiyo siyo lugha ya watu wenye hadhi; hata kama
matumizi ya lugha hiyo ya Kiswahili siyo sahihi, hilo halijalishi kwani
inakosewa lugha isiyo ya lazima kwao.