Monday 19 January 2015

150 WAPEWA MIMBA NA WANAFUNZI WENZAO CHUONI



Wanafunzi 150 kati ya 1,000 waliojiunga na masomo katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce) mwaka jana wamebainika kuwa na ujauzito waliopewa na wenzao chuoni hapo.

Utafiti wa usawa na jinsia uliofanywa na chuo hicho kati ya Juni na Novemba mwaka jana umebaini kuwa wanafunzi wanaopata ujauzito ni wale wa mwaka wa kwanza.

Hayo yamebainishwa jana na Mratibu wa Masuala ya Jinsia wa chuo hicho, Dk Dativa Shilla katika warsha ya uchaguzi na uhusiano wa kijinsia iliyofanyika chuoni hapo.

Alisema hali hiyo inatokana na kuwapo kwa vitendo vya ukatili, manyanyaso na ubabe unaofanywa na wanachuo wa kiume dhidi ya wale wa kike na hivyo kuwalazimisha kufanya mapenzi bila hiyari yao.

“Kupitia utafiti huu tumeona hakuna usawa wa kijinsia wa kupata elimu baina ya mwanamke na mwanamume kwa sababu mwenye ujauzito hawezi kufanya vizuri katika masomo yake ukilinganisha na mhusika wa kiume,” alisema.


Awali, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Amon Katunzi alisema ni wakati sasa kwa Serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wote kwa sababu hatua hiyo itapunguza wanafunzi wa kike kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi kwa sababu watakuwa na fedha za kujikimu.

“Lengo la warsha hii ni kutoa elimu na ushauri kwa wanafunzi wa jinsi zote ili waweze kusoma vizuri na kuacha ushawishi wa kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi. Pia, tunawashauri hata wale ambao wapo katika ndoa wavumilie na kuepuka kupata ujauzito ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao,” alisema Katunzi.

Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho Gosbeth Kihanga ambaye alikiri kuwapo kwa vishawishi chuoni hapo na kudai kuwa inachangiwa na ugumu wa maisha hasa kwa wanafunzi wa kike.

Alisema kupitia kongamano hilo wamejifunza na kuelewa mengi hususani katika suala la kupanga na kugawana majukumu, kubadilisha mtazamo na kuacha kutumia ubabe katika uhusiano wa mapenzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment