Monday 12 January 2015

JK: ELIMU BURE MWAKANI TANZANIA



Rais Jakaya Kikwete ametangaza habari njema kwa Watanzania kwamba kuanzia mwaka kesho, elimu ya msingi na sekondari itatolewa bure.

Alitangaza azma hiyo ya serikali juzi, wakati akizungumza katika karamu aliyowaandalia mabalozi ya  kuukaribisha  mwaka  2015 iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Alisema hatua hiyo inakuja baada ya serikali kukamilisha  sera mpya ya elimu na ufundi ili kuboresha sekta hiyo ambayo imepitishwa na  Baraza la Mawaziri.

Hatua hiyo inachukuliwa katika kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata kiwango hicho cha elimu kwa gharama inayobebwa na serikali.

“Kwenye sera mpya, imeainisha jinsi ya utoaji wa elimu bora na viwango vinavyokubalika katika ufundi, hii itawezesha  elimu hizi mbili kukidhi matakwa katika soko la ajira pamoja na kujiajiri,” alisema.

“Wazo hili la kufanya elimu hii kuwafikia kila mmoja sasa ndilo jukumu lililo mbele yetu tukianza na maandalizi ya kuhakikisha tunalitimiza lengo hili kuu kwa ufanisi mkubwa,”alisema.


Hatua ya Rais ya kutangaza azma ya  kutoa elimu bure, imekuja miaka 10 baada ya wapinzani hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kueleza kuwa, moja ya mikakati yao ni kutoa elimu bure kwa kila Mtanzania iwapo watachaguliwa kuongoza  taifa.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, aliwahi kutamka katika moja ya mikutano ya hadhara kuwa  chama hicho kimejiwekea ajenda nne na kuwa ifikapo 2015 kikishika dola, kazi yao ni kutoa elimu bure na bora kwa Watanzania.


Kwa upande wa kutoa elimu bure barani Afrika, Kenya ni mojawapo ambapo imeanza kuwapa wananchi wake elimu hiyo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuingia madarakani.

Kuhusu walimu, Rais Kikwete alisema mwaka uliopita katika kuhakikisha elimu ya sekondari inaboreshwa,  walimu 36,339  waliajiriwa na kubakisha  upungufu wa walimu 45,233 wa shule za msingi na sekondari ambao wataendelea kuajiriwa.

Alisema katika mkakati wa kuimarisha shule za kata katika masomo ya sayansi, ujenzi wa maabara umekamilika kwa asilimia 40.5 na ujenzi unaendelea.

Kwa upande wa ukuaji wa uchumi, Rais Kikwete alisema unatazamiwa kukua kwa asilimia 7.4 mwaka jana ikilinganisha na asilima  7.3  mwaka jana.

Alisema kutokana na ukuaji huo, Tanzania imekuwa miongoni mwa  nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi duniani.

Hata hivyo, alisema mfumko wa bei umepungua kufikia asilimia 4.8 mwezi uliopita kutoka asilimia sita iliyorekodiwa siku za nyuma.

Aliwaambia waalikwa  kuwa hali hiyo imetokana na kuongezeka kwa uzalishaji  chakula, ambapo mpaka mwezi uliopita  ziada ya nafaka  ilifikia tani milioni 3.25.

“Mafanikio haya yamekuja baada ya kutekeleza mipango yetu ya Kilimo Kwanza na mradi wa  Ukanda wa Kusini wa Kilimo,  Sagcot,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete, aliwaambia mabalozi hao kwamba  pato la taifa  (GDP) limefikia shilingi trilioni 70  mwaka 2013 kutoka shilingi bilioni 53.7 mwaka 2001.

Chanzo: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment