Sunday 4 January 2015

UKIPUNGUA, 'MINYAMA UZEMBE' HUENDA WAPI?

Kuwa na mwili wenye unene wa kupindukia ni tofauti na kuwa na uzito mkubwa kuliko kawaida ingawa watu wengi huchanganya mambo haya mawili na kufikiri kuwa ni jambo moja.

Unene wa kupindukia unatokana na kuwa na mafuta mengi mwilini ambayo yanasababisha mtu kuwa na nyama nyingi ambazo wengine huziita “minyama uzembe” na kitambi.

Lakini uzito mkubwa wa mwili unaweza kutokea pale mtu anapokuwa na misuli mikubwa, mifupa mikubwa, maji mengi mwilini pamoja na mafuta. Baadhi ya magonjwa na matumizi ya dawa pia yanaweza kuchagia mtu kuwa na uzito mkubwa.

Watu wenye tatizo la tezi shingo linalofanya kazi zake chini ya kiwango wanaweza kukabiliwa na tatizo hili. Matumizi ya dawa kama vile baadhi ya vidonge vya uzazi wa mpango na dawa za magonjwa ya akili, pia yanaweza kusababisha tatizo la mwili kuwa na uzito mkubwa.

Wanasayansi wa afya wamekuwa wakieleza kuwa kuna uhusiano mkubwa na wa karibu sana kati ya unene wa kupindukia na magonjwa ya moyo, kiharusi, kupanda kwa shinikizo la damu, saratani za aina mbalimbali, kisukari, kukoroma wakati wa usingizi, maumivu ya mgongo na uvimbe wa maungio yaani baridi yabisi. 
Kutokana na kupendelea kuwa na umbo la kuvutia na sababu za kiafya, watu wengi hulazimika kupunguza unene na uzito wa miili yao.

Lakini maswali ya msingi ambayo watu wengi wamekuwa wakijiuliza kuhusu kupungua kwa unene wa mwili ni pamoja na njia ipi iliyo bora ya kupunguza uzito au unene?


Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali wa lishe, njia bora na salama ya kupunguza unene na uzito ni ulaji unaozingatia kanuni za afya na lishe bora kwa kujiepusha na vyakula vyenye sukari nyingi na mafuta mengi.

Njia nyingine ni kufanya mazoezi kila siku na kujishughulisha na kazi mbalimbali zinazohitaji matumizi ya nguvu.

“Mazoezi ya kukimbia yanamsaidia mtu kujenga pumzi, kuondoa maradhi madogo madogo na kupunguza uzito,” anasema Mwalimu wa mazoezi Chiko Yosia.

Mwandishi wa habari anayeandika masuala ya mazoezi wa Gazeti la Mwananchi, Maimuna Kubegeya akizungumzia aina ya mazoezi yanayofanya mtu kuwa na umbo dogo anasema: “Unatakiwa kufanya mazoezi angalau kwa saa mbili kila siku, ili kupunguza mara mbili ya kiasi cha mafuta uliyokula katika siku.”

Ingawa wataalamu wengi wamekuwa wakitoa ushauri wa lishe na mazoezi kwa ajili ya kupunguza unene, utafiti wa hivi karibuni uliofanyika huko Australia umebaini kuwa wengi wao hawajui wapi mafuta yanayo sababisha ‘minyama uzembe’ yanapokwenda wakati mwili unapopunguza unene.

Zaidi ya asilimia 50 ya wataalamu 150 walioshiriki katika utafiti huo, hawakujua wapi ‘minyama uzembe’ inapokwenda.
Madaktari na wanasayansi wengi wamekuwa wakifikiri kuwa nyama za mafuta zinazopungua hugeuzwa kuwa nguvu na nyingine huyeyuka wakati zinapozalisha joto.

Lakini watafiti wa masuala ya kupungua kwa unene hivi karibuni wameibuka na ushahidi tofauti wa kisayansi kuhusiana na jambo hili. Katika utafiti huo wamebaini kuwa kiungo muhimu mwilini kwa ajili ya kupunguza unene ni mapafu.

Utafiti wao ulichapishwa katika jarida la afya la Uingereza la The British Medical Journal toleo la 349, Desemba mwaka 2014.

Mtaalamu wa Fizikia, Ruben Meerman akishirikiana na Mkuu wa Kitivo cha Sayansi za Bayoteknolojia na Baiomolekula, Profesa Andrew Brown wa Chuo Kikuu cha New South Wales, Australia, wanasema kiasi kikubwa cha mafuta yanayosababisha unene ni hewa ya ukaa ambayo hutolewa nje kwa njia ya mapafu pale tunapopumua wakati wa mazoezi na kazi ngumu.

Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa kwa kila kilo 10 za mafuta, kiasi cha kilo 8.4 hugeuzwa kuwa hewa ya ukaa ambayo hutolewa nje kwa njia ya kupumua na kiasi cha kilo 1.6 huwa maji ambayo hutolewa nje kama jasho, mkojo na majimaji mengine ya mwili.

Utafiti huo unaongeza kusema kuwa unene hutokea pale kiasi kikubwa cha wanga, sukari na protini zitokanazo na vyakula tunavyokula vinapogeuzwa kuwa triglycerides. Hizi hutengenezwa kwa kaboni, haidrojeni na oksijeni kisha huhifadhiwa katika seli za mafuta.

Ili kupunguza unene, ni lazima kusambaratisha muunganiko wa vimeng’enywa vinavyofanyiza ‘triglycerides’.

Katika utafiti huo pia ilibainika kuwa ili kupunguza kilo 10 za mafuta ni lazima kuvuta hewa safi ya oksijeni kiasi cha kilogramu 29 na kwamba mchakato huo huzalisha kiasi cha kilo 28 za hewa ya ukaa na kilo 11 za maji.

“Hakuna kitu kigeni katika elimu hii ya kemikali za mwili, lakini kwa sababu zisizojulikana inaonekana kwamba hakuna mtu aliyewahi kufikiria juu ya kufanya hesabu za kukokotoa kiasi hiki,” wanasema watafiti hao. 
“Watu hawawezi kubaini kiasi cha hewa ya ukaa kwa vile haionekani kwa macho wakati tunapopumua,” anasema Meerman mmoja wa wanasayansi waliofanya utafiti huu.

Hata hivyo, watafiti hao wanaonya kuwa kupumua kwa nguvu bila kufanya kazi ngumu au kufanya mazoezi hakuwezi kusaidia kupunguza unene kwa vile hakuwezi kuvunja muunganiko wa vimeng’enywa vinavyohifadhiwa katika seli za mafuta yanayotengeneza minyama uzembe na kuzalisha hewa ya ukaa.

Kupumua kwa nguvu pekee kunaweza kusababisha kizunguzungu, kiherehere cha moyo na kupoteza fahamu kutokana na kukosekana kwa ulinganifu wa kemikali za mwili kwa kuingiza mwilini oksijeni nyingi kuliko kiasi cha hewa ya ukaa inayozalishwa.

“Kwa kufanya mazoezi madogomadogo ya kukimbia kwa muda wa saa moja badala ya kubweteka kwa saa moja, utendaji wa mwili kushughulikia mafuta huongezeka mara saba zaidi na kuondosha kiasi cha gramu 40 za kaboni mwilini.
Hiyo pia husababisha kuongezea kwa uwezo wa mwili wa kuondosha kaboni kwa asilimia 20 hadi kufikia kiasi cha gramu 240 kwa siku moja,” inasema sehemu ya utafiti wa Ruben Meerman na Profesa Andrew Brown.

Utafiti huo unatoa angalizo kuwa kiasi kikubwa cha kaboni zinazopotea wakati wa kupunguza unene zinaweza kurudi mwilini kwa njia ya kula vyakula na kunywa vinywaji vyenye sukari nyingi.

“Kupunguza unene ni jambo linalohitaji kupunguza kiasi cha kaboni unazoingiza mwilini kwa njia ya kula kuliko zile unazotoa mwilini kwa njia ya kupumua,” wanasema watafiti hawa.

Ingawa utafiti huu unatoa ushahidi mpya juu ya uelewa wa namna mwili unavyopunguza unene, njia za kuupunguza zinabakia kuwa zilezile zinazofahamika kwa muda mrefu ambazo kwa ufupi ni kupunguza ulaji na kuongeza mazoezi ya mwili.
Chanzo: mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment