Sunday 18 January 2015

KISWAHILI NI CHA WASIOJUA KIINGEREZA?



Katika nchi nyingi za Afrika, jamii imejigawa katika jamii ndogondogo ziitwazo makabila.

Kila kabila linakuwa na lugha inayotambulisha jamii ile. Kwa kuwa katika nchi makabila ni mengi na yanaongea lugha tofauti ambazo mara nyingi hata hazisikilizani, nchi huamua kuweka lugha moja rasmi kuwa lugha ya taifa.

Wenzetu katika nchi nyingine waliamua kuchukua lugha ya wale waliowatawala kuwa ndio lugha ya taifa. Hivyo kama walitawaliwa na Waingereza lugha ya taifa inakuwa Kiingereza, kama walitawaliwa na Wafaransa basi lugha ya taifa inakuwa Kifaransa. Tanzania ni nchi moja katika nchi chache sana katika Afrika ambazo zinatumia lugha ambazo siyo lugha za walio watawala. Sisi Tanzania tunatumia Kiswahili kama lugha ya taifa.

Mimi najivunia sana lugha hii, ninatamba mbele za walimwengu kwamba sisi tuna lugha ya Kiswahili inayotuunganisha kama taifa. Pamoja na kwamba sasa Kiswahili kimeenea sehemu nyingine za dunia hii hasa zile za Afrika Mashariki bado mimi naona hiyo ni lugha yetu sisi na wengine wamejifunza kama sisi tunavyojifunza lugha za watu wengine.

Ninaamini wapo wenye fikira kama hizi za kwangu lakini ninahisi pia wapo wanaoona lugha hii haiwahusu. Wengi wa hao ni watu wanaojua Kiingereza ambao wanaona Kiingereza ndiyo utambulisho wa usomi.

Hivyo hata kama Kiswahili kinadidimia hilo sio tatizo kwao kwani hiyo siyo lugha ya watu wenye hadhi; hata kama matumizi ya lugha hiyo ya Kiswahili siyo sahihi, hilo halijalishi kwani inakosewa lugha isiyo ya lazima kwao.


Hebu fikiria wasomi tunaowategemea katika kutuonyesha namna bora ya kuenzi taifa letu ikiwa ni pamoja na kukienzi Kiswahili wameamua kutokienzi Kiswahili kabisa; kuongea kwao kunaonyesha kwamba Kiswahili hakina maneno ya kuelezea vitu, vitendo na mambo mengi hivyo wanaamua kuweka maneno ya Kiingereza badala ya Kiswahili. Jambo la ajabu wanapotakiwa kuongea Kiingereza kitupu hawawezi.

Wanapotakiwa kuongea Kiswahili wanachanganya. Sijui wasomi wetu ni wa taifa lipi lenye lugha hiyo yenye mchanganyiko wa Kiswahili na Kiingereza. Wapo wale wanaoona kwamba ukiongea kwa namna hiyo basi wewe ndiyo utaonekana umeendelea. Huu ni upuuzi wa hali ya juu. Upuuzi huu sasa unapelekwa hata kwa watoto wadogo wa sasa.

Utakuta baba anajua Kiswahili, mama anajua Kiswahili lakini eti mtoto anayeishi na kusoma nchi hii hii hajui Kiswahili. Wazazi wanahakikisha kwamba wanamtoa kabisa mtoto wao katika uwepo wa Kiswahili; watamsemesha Kiingereza, watamlazimisha aangalie vipindi vya televisheni vya Kiingereza, watahakikisha hachanganyi na watu wanaongea Kiswahili pekee.

Mwishowe, mtoto huyo anaamini kabisa lugha anayostahili kuongea ni Kiingereza na hiyo ya Kiswahili awaachie hao watu wasio na hadhi kama ya wazazi wake.

Sisemi kwamba watoto hao sasa wasijifunze Kiingereza, la hasha ni mimi niliwahi kuwahamasisha wanafunzi wahakikishe wanakijua Kiingereza kwa sababu wanapokwenda kufanya usaili katika sehemu za kazi wanazoomba ni Kiingereza ndiyo kinachotumika, pia lugha ya mawasiliano katika taasisi nyingi za watu binafsi hasa zile za watu wa nje ya nchi ni kiingereza na kama hawatafanya bidii ya kujua lugha hiyo kuna hatari ya kukosa kasi katika taasisi hizo.

Hata hivyo, hilo haliimaanishi kwamba sasa waiache lugha yao na kujifunza kiingereza peke yake. Huo ni utumwa wa hali ya juu. Huyo Mwingereza anakuja katika nchi hii kujifunza Kiswahili lakini bado anabaki na Kiingereza kama lugha mama na kamwe haiachi. Sasa sisi tunaofundisha watoto wetu kukiacha Kiswahili na kujibadilisha Waingereza tuna matatizo gani?

Kwa sasa Kiswahili kinaharibiwa hata na vyombo vya habari. Kuna matumizi yasiyo sahihi katika maneno kadhaa na leo tuangalie neno la ‘kuweza’. Neno hili linatumiwa visivyo na vyombo vya habari hata inafikia kuonekana kama matumizi hayo ni sahihi kabisa.

Unasikia mtangazaji wa redio au televisheni anasema “katika ajali hiyo watu watatu waliweza kupoteza maisha” unabaki kujiuliza ina maana hao waliofariki walifanya juhudi za kufariki hatimaye wakafanikiwa kufariki? Au utasikia “kutokana na mvua hiyo kubwa nyumba tano ziliweza kubomoka”.

Utafikiri nyumba hizo ziliweka lengo na mikakati ya kubomoka halafu zikajitahidi mpaka kweli zikabomoka. Kwani nini maana ya kuweza?. Wataalam wa lugha watusaidie katika hili.

Ninavyojua, neno hili linaweza kutumika katika watu wenye dhamira ya jambo hilo kutokea na wakalifanyia juhudi ya kutokea kama “wanafunzi wameweza kufaulu kwa alama za juu”, inaonyesha kwanza kuna nia ya kufanya hicho kitu halafu kunakuwa na kitendo cha kufanya hicho kitu na kinapokamilika tunasema ameweza kufanya kitu hicho. Sasa hili la mtu kuweza kupoteza maisha au nyumba kuweza kubomoka linatoka wapi?

Mbona neno hili linaendelea kutumika siku hadi siku na watangazaji wetu wanazidi kulizoea tu na kuona ni sahihi kabisa? Je ina maana wahusika kwa maana ya wahariri na waandishi wenyewe hawalioni hilo au wanaona ni sahihi kabisa kusema ameweza kupoteza maisha? Vyombo vya habari ni chanzo cha mafunzo ya aina nyingi ikiwemo matumizi sahihi ya maneno ya Kiswahili. Hebu fikiria mgeni anayetaka kujifunza lugha hii halafu anasikiliza vyombo vyetu vya habari, ni nini atajifunza?

Maeneo mengine ambayo yanapotosha kabisa Kiswahili ni maeneo ya matangazo mbalimbali hata yale yanayotoa maelezo ya mahali husika kama ofisi, barabara n.k. Unakwenda katika hospitali halafu unakuta kibao nje ya chumba kimeandikwa ‘incharge wa RCH’; sijui hii ni nini! Maana hapo kuna neno moja tu la Kiswahili yaani ‘wa’. Hivi kweli hakuna kabisa neno la Kiswahili kwa neno ‘incharge?

Watanzania hebu tuthamini Kiswahili kwa vitendo na kuwaonesha walimwengu kwamba hiyo ni lugha yetu. Mbona sisi hatupendi kuhodhi vitu au mambo? Wakisema Kiswahili kimetokea Kenya tunakasirika, tukitakiwa kuonesha uhalali wa Kiswahili kuwa chetu kwa kukiongea kwa ufasaha tunashindwa. Jamani tuamke kabla hatujaporwa hata lugha!


Chanzo: mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment