Friday, 27 February 2015

MTOTO ALIYETEKWA APATIKANA BAADA YA MIAKA 17


Celeste Nurse (in orange dress) and her husband Morne (in cardigan) leaving the Cape Town Magistrates Court on 27 Febraury
Celeste Nurse na mumewe Morne wana furaha hatimaye kumpata binti yao

Mwanamke mmoja Afrika kusini amefikishwa mahakamani kwa kumteka mtoto mchanga kwenye hospitali ya Cape Town miaka 17 iliyopita.

Wazazi halisi wa binti huyo, Celeste na Morne Nurse, walikutanishwa naye baada ya kujikuta kaanzishwa shule moja na dada yake.

Baada ya kuona namna walivyofanana, wazazi halisi wa familia hiyo walimwalika binti huyo kupata kahawa na hapo ndipo walipowasiliana na polisi.

Vipimo vya asidi nasaba vimethibitisha utambulisho wa binti huyo, ambaye amepelekwa ustawi wa jamii kwa sasa.

Bw Nurse alisema binti yake anapewa ushauri nasaha wa kina.

Mke wake alisema ni “kama ndoto” kumwona mtoto wake tena.

"Alipokutana na Cassidy [dada yake], kulikuwa na kitu kiliwavuta tu na ikaanzia hapo," aliiambia redio ya CapeTalk.

"Siku yake ya kuzaliwa ni tarehe 28 Aprili. Mwaka huu tunaweza kusherehekea naye. Itakuwa mara yetu ya kwanza naye na lazima tupange kitu kikubwa sana."

Ndugu wa anayedaiwa kumteka aliwaambia waandishi wa habari nje ya mahakama ya Cape Town: 
"Tumekuzwa na binti huyu, tumemtunza."

Mwanamke huyo aliyekamtwa na mumewe, hawana watoto wengine.

Mwanamke huyo, mwenye umri wa miaka 50, anashtakiwa kwa utekaji nyara, udanganyifu na kukiuka sheria ya Watoto, hivyo basi amedanganya kuwa yeye ni mama mzazi wa mtoto huyo, polisi walisema.

Kesi yake imeahirishwa mpaka tarehe 6 Machi.

MWIMBAJI MAARUFU RWANDA AFUNGWA MIAKA 10


 Rwandan musician Kizito Mihigo in April 2014

Mwimbaji maarufu wa Rwanda amepewa kifungo cha miaka 10 gerezani baada ya kukutwa na hatia ya kuwa na mpango wa kumwuua Rais Kagame na kuchochea chuki dhidi ya serikali.

Awali Kizito Mihigo alikiri kosa na kuomba msamaha, ikimaanisha hukumu yake imepunguzwa.

Mwenzake aliyetuhumiwa naye, Cassien Ntamuhanga, mkurugenzi wa kituo cha redio cha Kikristo, amefungwa kwa miaka 25 jela kwa kosa la ugaidi na uchochezi.

Aliendelea kukana tuhuma zote.

Mihigo alikiri kuwasiliana kwa ujumbe mfupi wa simu na kundi la upinzani lenye makao makuu Afrika Kusini, la Rwanda National Congress (RNC).

Alifutiwa makosa ya ugaidi huku Ntamuhanga akifutiwa kosa la jaribio la kumwuua Rais Kagame.

Licha ya Mihigo kukiri makosa yote yanayomkabili, wakili wake baadae alisema kulikuwa hakuna ushahidi wowote wa kumtia hatiani.

Patrick Karegeya ni mmoja wa waanzilishi wa RNC, aliyekuwa mkuu wa ujasusi wa Rwanda ambaye aliwahi kuwa mshirika wa Rais Kagame.

Karegeya alikutwa amekufa nchini Afrika kusini mwaka jana huku washirika wake, familia na mamlaka za Afrika kusini zikiilaumu serikali ya Rwanda, iliyokataa kuhusika na mauaji hayo.

GAUNI LA LUPITA NYONG'O LA $150,000 LAIBIWA



 

Gauni rasmi lenye thamani ya $150,000 lililoshonwa rasmi na kampuni ya Calvin Klein, na kuvaliwa na muigizaji Lupita Nyong'o wakati wa tuzo za Oscars, limeibiwa Hollywood.

Gauni hilo, lililopambwa na lulu nyeupe 6,000, liliibiwa katika hoteli moja, Nyong'o alipokuwa nje ya chumba chake.

Mkenya huyo alishinda muigizaji msaidizi bora mwaka jana kutokana na filamu ya Twelve Years a Slave na alikuwa miongoni mwa watangazaji katika shughuli ya Jumapili.

Jarida la People limemtaja kuwa mtu mrembo duniani wa mwaka 2014.

Polisi Lt William Nash alisema gauni hilo linaonekana kuibiwa siku ya Jumatano jioni na maafisa wanachunguza kupitia kamera za CCTV.

Hakuna aliyekamatwa mpaka sasa.                   

Calvin Klein ambaye ni mbunifu wa mavazi hajasema lolote kuhusiana na tukio hilo.

Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu

Wednesday, 25 February 2015

SHERIA YA UISLAM YA 1912 YABADILISHWA AUSTRIA



Protesters hold banners during the demonstration under the slogan "New Islam Law? Not with us!" in front of the parliament building in Vienna, Austria, 24 February 2015

Bunge la Austria limepitisha mabadiliko yenye utata katika sheria ya zaidi ya karne moja kuhusu Uislam.

Muswada huo, ambao nusu yake una nia ya kupambana na msimamo mkali wa Kiislam, unawapa Waislamu ulinzi wa kisheria lakini kuzuia ufadhili wa kigeni kwa ajili ya misikiti na ma-imam.

Waziri wa Uhamiaji wa Austria, Sebastian Kurz, alitetea mabadiliko hayo lakini viongozi wa Kiislamu walisema nchi hiyo inashindwa kuwapa haki sawa.

Sheria ya mwaka 1912 iliifanya Uislamu kuwa dini rasmi Austria.

Imeheshimiwa sheria hiyo kwa muda mrefu kuwa mfano wa kusimamia Uislam barani Ulaya.

Utaratibu mpya, uliyopendekezwa kwa mara ya kwanza miaka mitatu iliyopita, unaheshimu sikukuu za kidini na mafunzo kwa ma-imam.

Lakini makundi ya Kiislam yalisema kuzuia ufadhili kutoka nchi za nje si haki kwani misaada ya imani za Kikristo na Kiyahudi bado inaruhusiwa.

Walisema sheria hiyo inaonyesha kutokuwa na imani kwa kiwango kikubwa na Waislam huku baadhi wakipanga kuipinga kwenye mahakama ya katiba.

Bw Kurz aliiambia BBC "Tunachotaka ni kupunguza ushawishi wa kisiasa na udhibiti wa nje na tunataka kuupa Uislam nafasi ya kuimarika kwa uhuru zaidi ndani ya jumuiya yetu ikiambatana na taratibu zetu za Ulaya.”

JAMAICA SASA KUHALALISHA BANGI



 Jah P., left, and Jah Henry, smoke marijuana from a chillum pipe in Kingston, Jamaica, Wednesday, Aug. 18, 1999.

Jamaica imefuta suala la kumiliki kiwango kidogo cha bangi kuwa ni uhalifu kwa matumizi binafsi.

Bunge la nchi hiyo limepitisha sheria iliyokuwa na mjadala mzito kuruhusu kumiliki hadi gramu 57 za ‘marijuana’.

Pia itaruhusu mamlaka husika kutathmini matumizi ya kitabibu na kisayansi wa mmea huo.

Marijuana inalimwa kwa kiwango cha juu Jamaica na ina mizizi ya kiutamaduni.

Kisiwa hicho kinadhaniwa kuwa kikubwa kwa visiwa vya Carribean kuuza marijuana nje – ambapo hujulikana pia kwa jina la ganja na cannabis Marekani.

Uamuzi wake wa kulegeza masharti ya matumizi ya bangi ndani ya taifa hilo kunaashiria kama makubaliano fulani ya kidunia.

Nchi tele za Latin America na Marekani – na hivi karibuni Alaska – wamehalalaisha matumizi ya bangi hizo katika miaka ya hivi karibuni.

DRC YAANZA MAPAMBANO NA WAASI WA KIHUTU



Democratic Republic of Congo regular army soldiers stand guard in the Nakabumbi area of Kimbumba, 20kms from Goma, near the border with Rwanda, on June 14, 201

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeanza mashambulio dhidi ya waasi wa Kihutu wa Rwanda mashariki mwa nchi hiyo.

Awali mawaziri waliahidi kupambana na wapiganaji wa FDLR baada ya kushindwa kufika makataa ya kusalimisha silaha zao mwezi uliopita.

Waasi wa Kihutu walihusika katika mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.

Majeshi ya kutunza amani ya Umoja wa Mataifa DRC ilijitoa kuunga mkono harakati hizo kwasababu ya majenerali wawili wa serikali wanatuhumiwa kukiuka haki za binadamu.

Mashambulio hayo ya Jumanne yalifanyika mashariki mwa Congo katika jimbo la Kivu ya Kaskazini, takriban kilomita 10 kutoka kwenye mpaka na Burundi, jeshi hilo lilisema.