Monday, 8 December 2014

MFANYAKAZI WA NDANI AKIRI KUMBAMIZA MTOTO, UGANDA



Woman feeds baby

Mfanyakazi wa ndani nchini Uganda ambaye video yake ilipatikana kwa siri akimbamiza na kumpiga mateke mtoto mdogo amekubali kosa la kumdhalilisha mtoto.

Jolly Tumuhirwe, mwenye umri wa miaka 22, alishtakiwa mahakamani kwa kumtesa mtoto wa kike wa miezi 18.

Video ikionyesha utesaji wa mtoto huo ulizua tafrani kubwa iliposambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Baba yake mtoto huyo, Eric Kamanzi, aliweka kamera baada ya kugundua mtoto wake akiwa na majeraha na anaburuza mguu.

Mwendesha mashtaka wa serikali Joyce Tushabe aliiambia mahakama kuwa mfanyakazi huyo “anajutia” na kuomba msamaha.

Video hiyo iliyochukuliwa na kamera iliyokuwa imefichwa pembezoni mwa ukumbi, inamwonyesha Tumuhirwe akimpiga mtoto huyo alipokataa kula kisha akamtupa chini kwenye sakafu, huku akimpiga na tochi kabla ya kumkanyaga na kumpiga mateke.

Baada ya kunasa ukatili huyo, baba wa mtoto huyo aliripoti tukio hilo kwa polisi Novemba 13.

Tumuhirwe, ambaye hakuwa na wakili mahakamani, sasa anakabiliwa na miaka 15 jela kwa uhalifu huo.

Wakili wa serikali ameomba kesi hiyo iahirishwe siku ya Jumatatu ili aweze kukusanya ushahidi zaidi.

Hukumu ya Tumuhirwe itatolewa Desemba 10.      

Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na mwandishi wetu               

No comments:

Post a Comment