Sunday 28 December 2014

RUSHWA, NGONO TATIZO MISS TANZANIA

Mkurugenzi wa Lino Agency International, Hashim Lundenga

Serikali imesema imeyafungia mashindano ya Miss Tanzania baada ya waandaaji kukiuka taratibu na kanuni huku pia yakitajwa kukithiri kwa rushwa ya ngono na upendeleo.

Mashindano hayo yalifunguliwa mwaka 1994, yamefungiwa kwa miaka miwili baada ya kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi na washiriki.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Bazara la Sanaa Tanzania (Basata), Godfrey Mngereza alisema jana kuwa Kamati ya Miss Tanzania kupitia kampuni yake ya Lino Agency, imekiuka kanuni na taratibu zinazoongoza mashindano hayo.

“Ni kweli kwamba tumeifungia Miss Tanzania kwa miaka miwili, lakini haya si maazimio ya tathmini iliyofanyika mapema mwezi huu, bali kulikuwa na vikao mbalimbali vilivyofanyika na si kimoja, ni uamuzi mgumu ambao umekuja kutokana na sababu maalumu,” alisema Mngereza.


Imeelezwa kuwa maazimio ya tathmini ya mashindano hayo yaliyofanyika Desemba 12, mwaka huu hayakufikia uamuzi, bali vikao mbalimbali vilivyoendeshwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kwa kushirikiana na Basata ndivyo vilivyofikia hatua hiyo ili kutoa nafasi kwa waandaaji kujipanga upya.

Mngereza alisema baraza limegundua kuwa baadhi ya washiriki walichaguliwa kwa upendeleo bila ya kuwa na sifa zilizowekwa.

“Katika tathmini yalitolewa pia mambo mengi ikiwamo warembo kudaiwa kutumiwa kingono hili ni suala lisilo jema. Hakuna utaratibu maalumu wa kufanya usaili kwa warembo, hivyo wanaopita, wanapita kwa njia zisizo halali tangu vitongoji mpaka ngazi ya fainali,” alisema Mngereza.

Aliongeza kuwa tangu mwaka 2006 namna ushindi unavyopatikana umekuwa ukilalamikiwa, kwamba wanapewa watoto wa viongozi serikalini na wenye uwezo kifedha.

“Kwa mfano mwaka huu walikuwa wakitetea majibu yasiyo sahihi, hatimaye kamati ikasema kwamba cheti cha Sitti Mtemvu walichotuletea ni sahihi, sasa ninajiuliza wewe unawezaje kusema cheti ni sahihi huku hujadhibitisha,” alisema na kuongeza:

“Ndicho kilichojitokeza katika tathmini, alitakiwa kuwasiliana na mamlaka husika, kama ni mtihani kuna Necta na kama cheti cha kuzaliwa kuna Rita, kwa hiyo wasingengoja wadau wapige kelele, waandishi wa habari wamkalie kooni kwa kulisimamia hili ndipo utekelezaji ufanyike.”

Lundenga: Sina taarifa na kifungo

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Lino Agency International, Hashim Lundenga  aliliambia gazeti hili kuwa hajapokea barua yoyote kutoka wizarani wala Basata, huku akilaumu taarifa zilizotolewa kabla hajapewa barua rasmi.

“Sijapokea barua yoyote kutoka Basata na wala sijaitwa huko tangu ifanyike tathmini Desemba 12 ambapo tuliambiwa kwamba kamati ingepewa maazimio, lakini kabla ya kukabidhiwa barua na vitu vingine tunaona kwenye vyombo vya habari kwamba tumefungiwa,” alisema Lundenga na kuongeza:

“Tumefanya Miss Tanzania kwa miaka 21 na hatujawahi kuingia katika misukosuko kama ilivyokuwa kwa mwaka huu, unajua bwana wakati mwingine akufukuzaye hakwambii toka, hivi vitu vinakwenda kwa utaratibu na siyo hivyo.”


Chanzo: Mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment