Mamlaka za Marekani zimemkamata Mmarekani nchini Uganda kwa madai ya kuendesha mtandao wa kimataifa wa biashara ya fedha bandia.
Ryan Gustafson, mwenye umri wa miaka 27, alifunguliwa mashtaka ya kufanya njama na biashara ya fedha bandia nje ya Marekani baada pesa hizo kutumika katika biashara mbalimbali Marekani.
Shirika la kijasusi la Marekani limefuatilia pesa hizo na kugundua ziko Kampala, ambapo wanasema wamekuta mtandao unaotengeneza pia euro, rupia za India, franca za Congo na fedha nyingine bandia za kiafrika.
Mshukiwa huyo anakabiliwa na miaka 25 jela.
Mikono bandia, alokuwa akitumia mshukiwa kama glovu kuficha alama za vidole |
"Tutawawajibisha wahalifu wa mitandao mpaka haki ipatikane hata waishi wapi," Mwanasheria Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ya Pennsylvania David Hickton aliandika kwenye taarifa yake.
Pesa bandia ziligundulika Pittsburgh, Pennsylvania, katika maduka ya rejareja na biashara nyingine.
Maafisa wa kijasusi waligundua fedha hizo zilikuwa zikitumwa kutoka Uganda.
Alama ya kidole kwenye moja ya mizigo ikawaongoza mpaka kwa Bw Gustafson, raia wa Marekani ambaye awali alikuwa akiishi Texas.
Mamlaka za Marekani zinakadiria mshukiwa huyo alisambaza takriban dola milioni 2 katika soko la biashara ambazo zilikuwa bandia.
No comments:
Post a Comment