Sunday, 7 December 2014

ZARI 'THE BOSS LADY' ANAVYOWIKA TANZANIA

 
Wengi tunamfahamu kama Zari The bossy lady lakini jina lake halisi ni Zarinah Hassan mwanamuziki wa Uganda ambaye ameweka makazi yake nchini Afrika Kusini.

Licha ya kuwa kwenye tasnia ya burudani kwa muda mrefu, lakini umaarufu wake umeongezeka maradufu tangu alipoanza kuwa karibu na mwanamuziki Diamond Platinumz.

Ukaribu baina ya nyota hao umezua maswali mengi hasa baada ya kuzagaa kwa picha zao zinazowaonyesha wakiwa kwenye mapozi yenye utata.

Pamoja na kuwa wenyewe wamekanusha kuwa na uhusiano wa kimapenzi na kudai kuwa kuna kazi ya sanaa wanaifanya pamoja lakini vyombo vya habari vimekuwa vikiwamulika.

Kana kwamba hiyo haitoshi, siku za hivi karibuni mrembo huyu wa Uganda ameonyesha kuzidi kuwa karibu na Diamond katika shughuli mbalimbali ikiwemo kwenye hafla ya utoaji tuzo za muziki za Channel O zilizofanyika nchini Afika Kusini.


Kutokana na tuhuma hizo Zarinah amekuwa miongoni mwa mastaa ambao wamepamba kwenye vyombo mbalimbali vya habari katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Nyota huyu aliyezaliwa Septemba 23,1980 katika mji wa Jinja alianza kuonyesha mapenzi yake kwenye muziki tangu akiwa shule ya msingi ambapo alishiririki katika mashindano mbalimbali kuiwakilisha shule yake.

Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari Zari alikwenda nchini Uingereza kwa ajili ya kuendelea na masomo ya chuo ambako alichukua stashahada ya masuala ya vipodozi.

Licha ya kupata taaluma hiyo, akili na mawazo yake yote bado yalikuwa kwenye muziki na mwaka 2007 alifanikiwa kurekodi wimbo wake wa kwanza ulioitwa Oliwange.

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa safari ya muziki kwa mwanadada huyo ambaye amekuwa miongoni mwa wanawake walioweza kuipeperusha vyema bendera ya Uganda kupitia muziki.

Sambamba na kujihusisha na muziki, nyota huyu anatajwa kuwa na utajiri mkubwa kutokana na kujihusisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali.

Miongoni mwa biashara hizo ni pamoja na duka kubwa la vipodozi lililopo mjini Pretoria Afrika kusini pamoja na chuo cha ufundi kwa ngazi ya tatu.

Chanzo: mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment