Saturday 13 December 2014

MPAKISTAN ALIYEVUSHA WANYAMA HAI TZ ASAKWA


 

SHIRIKA la Polisi la Kimataifa (Interpol) sasa limemtaja rasmi raia wa Pakistani, Ahmed Kamran (32), aliyehusika na usafirishaji wa wanyama hai kama twiga hapa nchini, kama mmoja wa wahalifu wanaotafutwa zaidi duniani, Raia Mwema limebaini.

Mhalifu huyu alitoroka nchini mwaka 2011 wakati akiwa nje kwa dhamana na gazeti hili limebaini kwamba mtandao wa ujangili uliopo ndani ya vyombo mbalimbali vya serikali ndio uliomtorosha ili asitoe siri zake.

Ripoti ya mwezi uliopita ya Interpol ambayo gazeti hili limefanikiwa kuiona, imeeleza kwamba Kamrani anatafutwa kwa udi na uvumba na inahisiwa anaweza kuwa katika mojawapo ya nchi za Kenya, Pakistani au Qatar.

Ripoti hiyo imemnukuu mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa Interpol wanaohusika na ufuatiliaji wa wahalifu waliotoroka, Ioannis Kokkinis, akisema tatizo kubwa wanalolipata ni kuwa hakuna picha inayofahamika ya Kamrani.

“Katika mambo haya ya ukamataji wa wahalifu, taarifa ambayo inaelezea kitu kidogo sana inaweza kuibuka kuwa muhimu na kufunua kesi nzima. Kwa mfano, hatuna picha ya Kamrani na kama tukiipata, unaweza kukuta wakaibuka watu wachache wanaomfahamu na mara moja tukampata. Tunaomba msaada kwa yeyote aliyewahi kumuona mhalifu huyu atupe picha yake,” alisema.

Taarifa hizi mpya zinazidi kuleta mshangao kuhusu raia huyu kwa vile aliwahi kufikishwa mahakamani hapa Tanzania na si rahisi kwamba Jeshi la Polisi halikuwahi kuweka kumbukumbu za picha zake.


Usafirishaji wafananishwa na Safina ya Nuhu kwenye Biblia

Interpol imelinganisha usafirishwaji huo wa wanyama na tukio la kwenye Biblia Takatifu ambapo Nabii Nuhu alisafirisha wanyama kupitia Safina ili kuwaokoa na gharika.

Hata hivyo, tofauti na Nuhu, Kamrani yeye alitumia usafiri wa anga (ndege) ambapo wanyama kama vile swala, nyumbu, tai, twiga na aina nyingine ambao kwa idadi walifikia 170, walisafirishwa kwa njia hiyo.

Interpol imetoa taarifa kwamba baadhi ya wahalifu walioshirikiana na Kamrani kwenye usafirishaji huo walidai kwamba twiga watatu walikufa wakiwa mahali walipohifadhiwa kabla ya kupelekwa uwanja wa ndege na ilibidi waende tena mbugani kukamata twiga wengine watatu ili kufidia wale waliokufa.

“Baada ya twiga wale watatu kufa, ilibidi twende tena kwenye eneo la hifadhi kukamata twiga wengine watatu na wanyama wengine ili tuweze kufidia wale waliokufa,” ripoti hiyo inasema ikinukuu ushahidi wa Maulid Hamisi.

Tukio hilo la utoroshaji lilifanyika Novemba mwaka 2011, na linaelezwa kama mojawapo ya matukio ya ajabu kuwahi kutokea katika ardhi ya Tanzania katika eneo la ujangili.

Kamrani inadaiwa ndiye aliyeongoza operesheni hiyo ambayo ilienda na vitisho dhidi ya wafanyakazi wa KIA waliotaka kuhoji kuhusu suala hilo, huku wengine wakitishiwa maisha na kufukuzwa kazi.

Thamani ya wanyama wote waliosafirishwa ilikadiriwa kufikia kiasi cha takribani shilingi milioni 181.

Kamran alihukumiwa kwenda jela miaka 60 Desemba 5 mwaka huu na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Kobelo, baada ya kupatikana na hatia ya makosa manne huku akiwa hayupo mahakamani.

Hata hivyo taarifa zilizopatikana mjini Moshi mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya hukumu ya Mahakama , zinadai kuwa kuna uwezekano mtuhumiwa huyo alitoroka nchini baada ya kurudishiwa kinyemela hati yake ya kusaifira iliyokuwa inashikiliwa na Polisi mkoani Kilimanjaro.

“Kuna tetesi tumepata kuwa Kamran aliondoka nchini akitumia hati yake ya kusafiria baada ya kurudishiwa na maofisa wanaofanya kazi ndani ya ofisi ya Kamanda wa Upelelezi wa Mkoa wa Kilimanjaro (RCO), kwa maelekezo kutoka viongozi wa juu wa serikali, ” kilieleza chanzo chetu.

Aidha, kwa kwa mujibu wa mtoa habari wetu, Kamran alitoroshwa nchini kutokana na msingi kuwa kesi yake ingegusa vigogo wengi wa serikali kuhusu ushiriki wao katika kusafirishwa kwa wanyama hao iwapo uthibitisho wa nyaraka alizokuwa nazo mtuhumiwa huyo ungewasilishwa mahakamani.

Taarifa hizo zinadai kuwa kuna uwezekano mtuhumiwa huyo alitoroshwa na mtandao wa watendaji wa juu wa serikali ulipo Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya Mahakama, na waendesha mashitaka wa serikali pamoja na Jeshi la Polisi.

“Kamran hakufanya utetezi wake mahakamani kwa sababu hakuwapo kama hatua hiyo ingefanyika basi serikali ingebaki uchi kutokana na nyaraka alizokuwa nazo Kamran kuhusu kusafirishwa kwa wanyama hao,” aliongeza mtoa taarifa huyo.

Kwa nyakati tofauti Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro aliimbia Raia Mwema kuwa Polisi wanashikilia hati ya kusafiria ya Kamran, ingawa Jeshi hilo halikuwahi kuionyesha hati hiyo hadharani hadi leo.

Katika hukumu yake hakimu Kobelo alisema kutokana na ushahidi wa upande wa mashitaka ilithibitika kuwa Kamran ndiye aliyekuwa wakala katika biashara hiyo na ambaye ndiye aliyewasafirisha wanyama hao kwa kutumia ndege kubwa ya Jeshi la Qatar Emir Air Foece.

“Ingawa ndege hiyo ilikuwa na vibali vyote halali vya kuingia nchini kwa safari ya kidiplomasia kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Kamran hakuwa na kibali cha kuwasafirisha wanyama hao,” alisema akiongeza kwamba Mahakama haikuweza kupata uthibitisho wake kama alikuwa na kibali.

Katika hukumu hiyo, hakimu Kobelo aliwaona washtakiwa wengine wanne, Hawa Mang’unyuka, Martin Kimath na Michael Mrutu kuwa hawana kesi ya kujibu na kuwaachia huru.

Kashfa hiyo ya kutoroshwa wanyama hai ni kati ya kashfa zilizotikisa nchi mwaka 2012 baada ya kuibuliwa na gazeti la Raia Mwema na tangu wakati huo watendaji kadhaa ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii wamepoteza nafasi zao na kufikishwa mahakamani.


Chanzo: raiamwema.co.tz

No comments:

Post a Comment