Tuesday, 2 September 2014

IS YATUHUMIWA KWA MAUAJI YA KIMBARI




 A member of the Iraqi Shiite militia, Kataib Hezbollah (Hezbollah Brigades), aims his rifle during fighting against Islamic State (IS) fighters, in Amerli town (1 September 2014)


Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International limesema lina ushahidi mpya kuwa wapiganaji wa Islamic State wamefanya mauaji ya kimbari kaskazini mwa Iraq.

Shirika hilo limesema kundi hilo la IS limegeuza eneo hilo kuwa “uwanja wa ukatili wa kumwaga damu”.

Awali Umoja wa Mataifa ulitangaza kutuma wataalamu Iraq kuchunguza “vitendo vinavyokiuka haki za binadamu kwa kiwango kisichofikirika”.

IS na waasi washirika wa Ki-Sunni wameteka maeneo makubwa ya Iraq na Syria.

Maelfu ya watu wameuawa, wengi wao wakiwa raia, na zaidi ya milioni wamelazimika kukimbia makazi yao katika miezi ya hivi karibuni.

Amnesty imesema imekusanya ushahidi kuwa kumekuwa na mauaji ya watu wengi yaliyofanyika kaskazini mwa mji wa Sinjar mwezi Agosti. Matukio mawili ya kutisha yalifanyika baada ya wapiganaji wa IS walipovamia vijiji na kuua mamia ya watu Agosti 3 na 15.

“Makundi ya wanaume na vijana wa kiume wakiwemo watoto wa chini ya miaka 12 kutoka vijiji vyote viwili walitekwa na wapiganaji wa IS, wakachukuliwa na kufyatuliwa risasi,” shirika hilo lenye makao makuu Uingereza limesema.

Naibu Kamishna wa haki za binadamu Flavia Pansieri ameonya IS (mwanzo ikijulikana kama ISIS) ilikuwa ikiwalenga Wakristo, Wayazidi, Wa-Shabak, Wa-Sabea na jumuiya za Kishia “kupitia mauaji ya kikatili kupita kiasi”.

Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment