Monday, 1 September 2014

KATIBA BADO KIZAAZAA, TANZANIA



Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana waligoma mbele ya Rais Jakaya Kikwete kuruhusu wajumbe wao kurejea katika Bunge Maalumu la Katiba, walipokutana katika kikao cha kusaka suluhu ya mkwamo wa mchakato wa Katiba.

Mkutano wa jana ulikuwa na sehemu mbili kuu, wa kwanza ulifanyika katika Ikulu ya Kilimani, Dodoma ambako viongozi hao walikutana na Rais Kikwete na mwingine katika Hoteli ya St. Gasper ambao uliwashirikisha viongozi na maofisa wa vyama vilivyoshiriki bila Rais Kikwete.

Mkutano huo ni matunda ya jitihada zinazofanywa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambacho kiliratibu mazungumzo hayo yaliyochukua zaidi ya saa mbili na nusu, katika Ikulu ya Kilimani, wakati yale ya St. Gaspar yalichukua takriban saa moja na nusu.

Viongozi walioshiriki kikao hicho cha Ikulu ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), Magdalena Sakaya.

Wengine ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Katibu Mkuu wake, Mosena Nyambabe, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, Mwenyekiti wa UDP ambaye pia ndiye mwenye zamu ya uenyekiti wa TCD, John Cheyo na Mwenyekiti wa UPDP pamoja na mwakilishi wa vyama visivyokuwa na wabunge ndani ya TCD, Fahmi Dovutwa.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Rais Kikwete baada ya kuanza kwa kikao hicho alitoa fursa kwa kila aliyekuwapo kuzungumza na hapo zilijitokeza hoja mbalimbali, nyingi mwelekeo wake ukiwa ni kutaka kusitishwa kwa Bunge Maalumu ili kutoa fursa kwa nchi kuendelea na masuala mengine makubwa.

Chanzo chetu kilisema: “Rais amekuwa msikivu kweli, amewasikiliza wote lakini ugumu ulianza kuonekana pale ilipotolewa kauli ya kuwauliza wale watu wa Ukawa kama wanaonaje wakirejea halafu hoja zao zikazungumzwa ndani ya Bunge Maalumu, yaani hawataki kabisa kusikia hilo.”

Kuhusu hoja ya kusitishwa kwa Bunge, habari zinasema ilijadiliwa kwa kirefu na wataalamu wa sheria wakijaribu kutoa uzoefu wao, lakini kikwazo kilichoonekana ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo haimpi Rais mamlaka ya kusitisha Bunge.

“Rais alisema hoja zao ni nzuri na zina mashiko, lakini suala kubwa likawa ni kwamba tunafikaje huko wanakopendekeza? Maana sheria iko kimya kuhusu mamlaka ya Rais kusitisha Bunge Maalumu, ndiyo maana sasa tulitoka Ikulu tukaenda St. Gaspar ili kujadili, ngoja tusubiri hiyo tarehe 8 maana siyo mbali,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.

Kwa taarifa zaidi, bonyeza hapa http://bit.ly/1vCIxPA

Chanzo: Mwananchi, Tanzania

No comments:

Post a Comment