Wednesday, 3 September 2014

MOTO WAKATIZA BIG BROTHER AFRIKA



Big Brother winner Cherise Makubale
Cherise Makubale wa Zambia alikuwa mshindi wa kwanza wa Big Brother Africa 



Uzinduzi wa mfululizo wa Big Brother Afrika umecheleweshwa kutokana na moto mkubwa uliotokea katika studio zao maalum mjini Johannesburg.

Kipindi hichi, kilichotarajiwa kuanza Jumapili, kimesimamishwa huku watayarishaji wanajaribu kutafuta nyumba mbadala “haraka iwezekanavyo”

Hakuna aliyejeruhiwa kwenye moto huo na sababu haitojulikana mpaka uchunguzi utakapofanyika.

Washindani kutoka nchi 14 walitarajiwa kushiriki kwenye kipindi hicho ikiwa ni cha tisa.

Kilitarajiwa kuwepo kwa siku 91 kabla ya kupata mshindi wa kumrithi yule wa mwaka jana Dilish Matthews kutoka Namibia.

Mshindi wa mwaka huu anatarajiwa kushinda dola za kimarekani 300,000, sawa na kiwango kilichotolewa mwaka 2013.

Watengenezaji wa kipindi hicho Endemol South Africa na M-Net wamesema jitihada za kutafuta jengo jengine ili kurekodi kipindi hicho itakuwa ngumu katika kipindi kifupi kutokana na “ubora wa miundo mbinu” ambayo haitopatikana haraka.

Kila jitihada itafanyika kutafuta suluhu haraka iwezekanavyo ili kipindi hicho kinachotazamwa na idadi kubwa ya watu Afrika kiendelee,” waliongeza.

Channel 24 imesema tayari matayarisho yalipatwa na mtikisiko baada ya washindani kutoka Ghana walipokabiliwa na matatizo ya kupata viza na badala yake kuchukuliwa Waghana ambao tayari ni wakazi wa Afrika Kusini.

Washiriki wa Rwanda- kwa mara ya kwanza- na Sierra Leone nao pia ilibidi wafutwe.
Kipindi hicho kipya kilitarajiwa kuonyeshwa kote barani Afrika kupitia satelaiti.

Big Brother imekuwa maarufu sana tangu ilipoanza mwaka 2003, na imepata washindi kutoka Tanzania, Angola, Nigeria, Namibia, Zimbabwe na Afrika Kusini.

Mshindi wa kwanza, Cherise Makubale, alitokea Zambia.

Mwaka 2010, kipindi hicho kilirindima kwenye vichwa mbalimbali vya habari duniani baada ya mmoja wa washiriki wa kiume  alipotolewa kwenye jumba hilo la Big Brother kwa kumpiga ngumi mshiriki wa kike.

Awali watengenezaji wa kipindi hicho nchini Afrika Kusini walimruhusu Hannington Kuteesa kubaki kwenye kipindi hicho, jambo liliosababaisha malalamiko mazito.

Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na mwandishi wetu
 

No comments:

Post a Comment